Shirika la Masoko ya Kariakoo linapenda kuwataarifu wananchi na wadau wote kuwa limefikia hatua za mwisho za maandalizi ya kuwarejesha wafanyabiashara katika Soko Kuu la Kariakoo kufuatia kukamilika kwa mradi mkubwa wa ujenzi na ukarabati wa soko hilo ulioanza mwaka 2022.
Akizungumzia hali ya maandalizi Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo Ashraph Abdulkarim ofisini kwake Dar es Salaam Juni 26,2025 alisema mradi huu umetekelezwa kwa mafanikio makubwa chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Serikali ilitoa shilingi Bilioni 28.03, imewezesha kukamilika kwa mradi huu wa kimkakati ambao unatarajiwa kuleta mchango mkubwa katika uchumi wa nchi kwa kuongeza fursa za biashara pamoja na ajira zaidi ya 4,000 kwa Watanzania kupitia Soko la Kariakoo ambalo litakuwa na nafasi za biashara 1,907.
Tangu kukamilika kwa zoezi la uhakiki wa wafanyabiashara waliokuwepo awali katika soko hilo, Shirika linaendele kuwapanga wafanyabiashara 1,520 pamoja na wale waliopata maeneo ya biashara kupitia mnada katika mfumo wa TAUSI kulingana na aina za biashara zao, na kazi ya upangaji inafanyika kwa kuzingatia usawa, uwazi na ufanisi.
Shirika linawashukuru wafanyabiashara wote kwa ushirikiano wao mkubwa, na tunatarajia kuendelea kushirikiana nao katika hatua inayofuata ya kurejea rasmi katika maeneo yao ya biashara ndani ya soko jipya la Kariakoo.
General Manager, Kariakoo Markets Corporation, Nyamwezi/Tandamti Street,
Postal Address: P. O. Box 15789 Dar es Salaam, Tanzania
Telephone: +255 22 2180678
Mobile:
Email: info@kariakoomarket.co.tz
Copyright ©2024 Shirika la Masoko ya Kariakoo . All rights reserved.